
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA, imewafikisha mahakamani watuhumiwa wanne kwa tuhuma za kusambaza ujumbe wa uongo katika mtandao wa kijamii wa Whatsapp, unaoelezwa kuzungumzia kubainika kwa masanduku ya kura bandia katika majimbo mbalimbali nchini.
Wakisomewa mashtaka watuhumiwa hao wanne Leila Costantine Sinare, Godfrey Edward Soka ,Deo Edmond Soka Pamoja na Monica Gaspery Soka katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu mbele ya hakimu Mkuu mfawidhi Cyprian Mkeha inadaiwa watuhumiwa hao walisambaza ujumbe wa uwongo na wa kupotosha katika mtandao wa whatsapp kwa njia ya sauti.
Akizungumza mara baada ya kesi hiyo Kaimu Mkurugenzi wa TCRA Joannes kaungura amesema watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani kufuatia kubainika kutenda kosa kinyume na sheria ya makosa ya mtandao iliyopitishwa mwaka huu.
Watuhumiwa hao wanne wametoka kwa dhamana baada ya kutimiza mashariki ya kuwa na mdhamini mmoja anayetambulika pamoja na shilingi milioni Tano, Kesi hiyo itatajwa tena Desenba 3,mwaka huu