Thursday , 23rd Apr , 2015

Utafiti uliofanywa na taasisi ya REPOA kupitia mradi unaofuatilia mitizamo ya jamii juu ya masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii barani Afrika - Afrobarometer, umeonyesha kuwa Watanzania bado wana imani na utendaji wa vyombo vya habari.

Matokeo ya utafiti huo yametolewa leo jijini Dar es Salaam, ambapo mtafiti wa REPOA ambaye ndiye msimamizi wa mradi huo Bi. Rose Aiko, amesema licha ya kuonesha imani na vyombo vya habari, watanzania wanataka mkazo zaidi uwekwe katika uandishi wa habari za kiuchunguzi ambazo zitaibua maovu pamoja na utendaji mbovu unaofanywa na serikali pamoja na taasisi zake.

Hata hivyo, Bi. Aiko amesema kumekuwa na maoni ya kushangaza kidogo kwani baadhi ya waliohojiwa katika utafiti huo, wametaka kuwepo kwa utaratibu ambapo serikali itakuwa ikisimamia utendaji wa vyombo vya habari nchini, hatua aliyodai kuwa inakwenda kinyume na matakwa ya kuwepo kwa uhuru wa habari na kujieleza, hususani uhuru wa vyombo vya habari.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji kutoka ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – Chadema, Victor Kimesera ameonyesha wasiwasi kuwa utafiti huo haukuangalia pia baadhi ya mambo ikiwa ni pamoja na undani wa mtazamo halisi wa Watanzania kuhusu uhuru wa habari nchini.

Amesema licha ya watanzania hao kuonesha kuridhishwa na utendaji wa vyombo vya habari, bado utafiti huo umeshindwa kueleza ni kwa nini watanzania hao hao hubaki kimya pale serikali inapovifungia baadhi ya vyombo vya habari kwa sababu ambazo hazina msingi.

Aidha, ameitaka REPOA kuangalia uwezekano wa kuangalia pia athari ya baadhi ya sheria kandamizi zilizopitishwa na bunge hivi karibuni ambazo amesema kimsingi zinanyima uhuru wa habari.

Amezitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni sheria ya takwimu pamoja na sheria ya makosa mtandaoni, ambapo kwa upande wa sheria ya makosa mtandaoni, mzee Kimesera amesema inakwenda kinyume kabisa na dhana ya upashanaji habari hasa kipindi hiki ambapo habari ni moja ya nyenzo muhimu katika kuchochea kasi ya ukuaji wa maendeleo.