Wednesday , 29th Jun , 2016

Baadhi ya wananchi mkoani Mtwara, wamewaomba wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja na kampuni za uwekezaji kusaidia kutatua changamoto za miundombinu katika hospitali na vituo vya afya ikiwa ni pamoja na kutoa vitanda kwa ajili ya wagonjwa na wauguzi.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akikagua neti ya mmoja wa mama aliyejifungua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Ligula.

Wakizungumza katika zoezi la kupokea msaada wa vitanda na gari la wagonjwa kutoka kwa kampuni ya Ndovu Resources Ltd, katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula, wamesema wauguzi wanapata shida wanapokua wodini kwa sababu wanalazimika kulala chini kwa kukosa vitanda.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya uchimbaji wa mafuta na gesi, Issaya Chialo, ameisisitiza juu ya matumizi mazuri ya vifaa hivyo, huku Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akishukuru kwa msaada huo pamoja na kuwataka watendaji katika vituo vya afya na hospitali pamoja na watumiaji kuvitunza vifaa hivyo.

Jumla ya vitanda 12 vyenye thamani ya sh. Milioni 50 vimekabidhiwa kwa ajili ya matumizi katika hospitali ya Ligula huku gari moja la wagonjwa lenye thamani ya sh. Milioni 40 likikabidhiwa katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara kwa matumizi ya kituo cha afya cha Nanguruwe.