
Gharama kubwa za matibabu kwa watu wenye ulemavu zikiwemo huduma za mazoezi na upasuaji zimefanya waendelee kuteseka kwa magonjwa yanayoweza kutibika huku serikali ikitajwa kutokuwa na fungu maalum la fedha katika halmashauri kwa ajili ya kusaidia watu wenye ulemavu.
Hali hiyo inafanya vituo vya walemavu kutegemea wahisani ambao wengi wao wameacha kutoa fedha katika vituo hivyo kama ilivyo kwa kituo cha walemavu Monduli ambacho kina idadi kubwa ya wagonjwa wasiyo na uwezo.
Mratibu wa kituo cha walemavu Monduli Mireille Kapilima ametoa kauli hiyo katika uchangiaji wa fedha kwa ajili ya kusaidia watu wenye ulemavu katika kituo hicho kinachohudumia walemavu zaidi ya 300 ambao wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa huduma za afya chakula na zingine baada ya wahisani kuacha kukisaidia kituo hicho na kudai kuwa huduma hizo zimekuwa juu hadi kufikia laki nne kwa huduma moja na wengi wa watu hao wakiwa wanatoka katika familia masikini.
Makamu Askofu wa kanisa katholiki jimbo kuu la Arusha Simon Tengesi amesema kuna haja ya watanzania kuanza kujitegemea kwa maswala ya kijamii kama kusaidia watu wenye ulemavu kwani wafadhili wengi wameanza kujitoa na serikali inatakiwa kuweka mipango madhubuti itakayo wezesha jamii zenye ulemavu kupata haki zao za msingi.
Kwa upande wao watoto wanaolelewa katika kituo hicho wamewataka watanzania na serikali iwaangalie kwa jicho la huruma kwakuwa walemavu ni binadamu kama wengine na kuunga mkono huduma zinazotolewa na kanisa katholiki katika kituo hicho huku afisa utumishi wa wilaya ya monduli Dominic Msagati akikiri kuwepo kwa ukosefu wa fungu za fedha kutoka serikalini katika idara ya ustawi wa jamii na kwamba imekuwa kikwazo katika utoaji wa huduma bora kwa watu walemavu.