Thursday , 15th May , 2014

Ikiwa ni siku tatu tu kupita tangu kutokea tukio la mauwaji ya mlemavu wa ngozi huko Simiyu Bariadi wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu ikiwemo mauaji ya walemavu wa ngozi.

Picha ya mtoto aliyezaliwa akiwa na ulemavu wa ngozi ujulikanao kama albinism.

Wakiongea katika mahojiana na East Africa Radio wakazi hao wamesema wanasikitishwa na vitendo vya mauaji ya walemavu wa ngozi na kueleza kuwa kuongezeka kwa matukio hayo kunatokana na kuzorota kwa ulinzi na usalama kwa jamii hii ya walemavu wa ngozi.

Baadhi ya wakazi hao ni Godfrey Swai Maso, Eliada James na Said Mdaka, ambao wamedai kuwa serikali haijachukua hatua za kutosha kukabiliana na wimbi la matukio hayo ya kikatili ambayo pia yanahusishwa na imani za kishirikina.

Kwa upande wake mlemavu wa ngozi Bi. Mariam Staford ambaye nae alivamiwa nyumbani kwake huko Kagera na kukatwa mikono yake miwili ameelezea kwa masikitiko vitendo wanavyofanyiwa watu wenye albinism huku akisema serikali imeshindwa kabisa kuwalinda.