Thursday , 17th Sep , 2015

Waandishi wa habari nchini, wametakiwa kuandika habari za ukweli, katika kipindi hiki cha uchaguzi na kuepuka uchochezi, ili taifa lisiingie katika machafuko.

Mkufunzi kutoka MCT,Chrysostom Rweyemamu.

Hayo yamesemwa leo Jijini hapa na Mkufunzi ,Chrysostom Rweyemamu wakati alipokuwa,kwenye warsha ya waandishi wa habari za uchaguzi wa Kanda ya Kaskazini, inayofanyika Jijini Arusha.

Amesema uandishi salama ni ule unaosimamia ukweli, bila kuegemea upande wowote na kukaa mbali na ushabiki wa vyama vya siasa.

Chrysostom amesema kuandika katika gazeti au kuripoti katika Televisheni au Radio, ni kusema ukweli kwa yale yanayotokea, lakini si kuongeza maneno kutoka kinywani mwa mgombea.

Naye mkufunzi mwingine, Paul Mallimbo amewasihi wanahabari kuhakikisha wanaacha tabia ya kuwapamba wagombea, badala yake wasimamie maadili ya taaluma zao ili waweze kuwa salama.

Amesema ni vyema wanahabari wakasoma sheria ya uchaguzi ya mwaka 1995 namba 8 na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 inayozungumzia jinsi ya kutotoa rushwa nyakati za uchaguzi, ikiwemo uadilifu badala ya kupamba chama kimoja.

Pia amesema ni vema kila mwandishi akazingatia kutoa matokeo ya Urais yanayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ili kujihakikishia kuwa salama.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamendaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) yamewakutanisha wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari kutoka Mikoa yaTanga, Manyara na Arusha.