Sunday , 2nd Nov , 2014

Mdahalo uliokuwa ukifanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini DSM umeshindwa kuendelea kutokana na vurugu zilizojitokeza ukumbini hapo.

Mdahalo uliokuwa ukifanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini DSM umeshindwa kuendelea kutokana na vurugu zilizojitokeza ukumbini hapo.

Mdahalo huo uliokuwa unahusu Elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa ulikuwa umeandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kushirikisha waliokuwa makamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji mstaafu Joseph warioba.

Jaji warioba ndiye aliyekuwa wa kwanza kuichambua Katiba inayopendekezwa, na kuelezea mapungufu kadhaa ikiwa ni pamoja na masuala ambayo Bunge La Katiba limeyaacha kutoka katika Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume hiyo.

Katika maelezo yake, Jaji Warioba ameeleza kusikitishwa kwake na kuachwa kwa mambo ya muhimu ikiwa ni pamoja na miiko ya uongozi pamoja na Tunu za Taifa, lakini amepongeza baadhi ya mambo kuboreshwa ikiwa ni pamoja na Haki za Binadamu.

Kuhusu muundo wa muungano, Jaji Warioba amesema kuwa muundo uliopendekezwa katika Katiba Inayopendekezwa haufai na kuwa unasababisha mgogoro mkubwa zaidi wa muungano, hasa katika suala la kiuchumi.

Amesema Katiba hii inasababisha kile kinachoitwa koti la muungano kimekuwa kikubwa zaidi zaidi, na kuna uwezekana mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yakashindikana hali inayoweza kuzalisha kuwepo kwa nchi mbili zenye Katiba tofauti ndani ya nchi moja.

Wakati akielezea umuhimu wa kuweka miiko ya uongozi kwenye Katiba, ndipo baadhi ya vijana wakatoa mabango yenye ujumbe wa kupinga hotuba ya Warioba na kuunga mkono katiba inayopendekezwa.

Bango mojawapo lilisomeka “TUMEIPOKEA, TUNAIKUBALI NA TUNAIUNGA MKONO KATIBA PENDEKEZWA”

Baada ya hapo kilichofuata ni vurugu zilizoambatana na mapigano miongoni mwao kati ya wanaounga mkono katiba na wanaopinga.

Mdahalo huo uliokuwa ukitangazwa moja kwa moja kupitia redio na televisheni ulivurugika kutokana na kundi la vijana wapatao 20 kuanza kumzomea aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipokuwa akiwasilisha mada yake.

Vijana hao ambao haijajulikana walitokea wapi au walikuwa na ajenda gani waliinua mabango ya kupinga msimamo wa waliokuwa wakiendesha mdahalo na kusema rasimu ya katiba iliyopendekezwa inakidhi mahitaji yote na kusema hakuna haja ya mdahalo.

Jaji Warioba ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania alifanikiwa kutoka nje ya ukumbi ulipokuwa ukifanyika mdahalo huo, lakini wapo watu waliojeruhiwa kutokana na kurushwa viti na vitu vingine.