Saturday , 20th Jun , 2015

Zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa kutumia mfumo BVR katika maeneo mengi ya mkoa wa Mara limeingia dosari baada ya mashine zinazotumika kushindwa kufanya kazi na kupelekea vituo vingi kufungwa.

Zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa kutumia mfumo BVR katika maeneo mengi ya mkoa wa Mara limeingia dosari baada ya mashine zinazotumika kushindwa kufanya kazi na nyingine kuharibika, hatua ambayo imesababisha vituo vingi kufungwa na kuibua malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

Kasoro hizo zimeripotiwa katika wilaya za Serengeti, Bunda, Butiama na Musoma mjini hatua ambayo imesabisha baadhi ya wananchi kushinda na kukesha katika vituo hivyo wakisubiri mashine hizo zitengenezwe.

Baadhi ya wananchi ambao wamefika katika vituo hivyo vya manispaa ya Musoma saa nane za usiku, wamesema kitendo cha kuharibika kwa mashine hizo kuna hatari kubwa ya kusabisha wananchi wengi kukosa haki ya kujiandikisha endapo tume ya taifa ya uchaguzi haitaongeza muda zaidi wa kujiandikisha.

Mkurugenzi wa manispaa ya Musoma mkoani Mara Dkt. Khalfan Haule, amekiri kutokea kwa kasoro hizo lakini amesema hivi sasa baadhi ya mashine zimetengenezwa na kurejeshwa katika baadhi ya vituo.

Baadhi ya wananchi waliokuwa wakisubiri kuandikishwa walianza kufanya shughuli nyingine kama kusukana hapo hapo vituoni