Friday , 14th Dec , 2018

Julai 28 mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli aliwateua kwa pamoja waliokuwa makada wa vyama vya upinzani nchini na baadaye kujiunga na Chama Cha Mapinduzi ambapo walipewa nafasi mbalimbali ikiwemo Ukuu wa Wilaya, Katibu Tawala.

Viongozi waliokuwa upinzani na baadaye kuhamia CCM.

Miongoni mwa viongozi waliopewa nafasi hiyo Julai 28 ni Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, David Kafulila ambaye alishawahi kuwa Mbunge Jimbo la Kigoma kusini kupitia Chama Cha NCCR Mageuzi mwingine ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA, BAVICHA pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Moses Machali.

Akizungumza na www.eatv.tv Kafulila alieleza kuwa anafurahia kazi aliyopewa na Rais Magufuli na kubainisha atahakikisha anaitendea kazi kama alivyokuwa wakati akiwa Mbunge wa Kigoma Kusini.

"Kazi yangu ya utendaji hasa zama za Magufuli imekuwa nyepesi kwa mtendaji mwaminifu, na hasa ukiwa mtendaji ambaye hupendi rushwa, mi nafurahia sana nipo kwenye utendaji, ningekuwa kwenye ubunge ningependekeza lakini mimi kama mtendaji ninatakiwa kufanya maamuzi.”Ameongeza Kafulila"

Kwa upande wake Patrobasi Katambi Decemba 02 mwaka huu akizungumza na www.eatv.tv alieleza atahakikisha anawachukulia hata baadhi ya wabunge ambao wataonekana kutotii sheria na taratibu za nchi pindi watakapofika kwenye wilaya yake.

"Mimi sijawahi kukutana na mbunge yeyote wa upinzani lakini kila wanapokuja Dodoma lazima wafuate sheria, na taratibu za nchi kwa sababu Dodoma ni makao makuu ya nchi, serikali na chama kinachoongoza dola kwa hiyo wanapokuwa hapa wafanye kazi za kibunge na si vitu vingine kwa sababu watakuwa chini yangu kama Mkuu wa wilaya." Amesema Katambi.

Moses Machali ambaye awali alikuwa mwanachama wa ACT alieleza juu ya hatma yake ya kuwania tena Ubunge ambapo alieleza kwa sasa kuwa hawezi kuizungumzia nafasi hiyo kutokana na kubanwa na taratibu za chama chao.

"Si kweli kwamba niko kimya sana, tatizo waandishi wa habari hawatutembelei kwa sababu wilaya yangu iko mbali sana kutoka Mtwara Mjini, na hata kama Spika alisema tutumie mitandao ya kijamii kujitangaza kazi zetu, Spika anajua kuna tofauti kati ya kazi za kibunge na Ukuu wa Wilaya."

"Kuhusu suala la kugombea tena ubunge kupitia CCM kwa sasa sina cha kusema, sitaongea kwa sasa kwa sababu nitakuwa nimekiuka misingi ya chama, kwa hiyo nahifadhi maneno yangu," amesema Machali.