Dkt Wilbroad Slaa akihutubia umati wa wananchi mjini Arusha
Dkt Wilbroad Slaa amesema UKAWA hawatakimbilia kugawana madaraka badala yake watapambana kupigania kuona wananchi wanapata katiba mpya itakayowakomboa.
Dkt Slaa ameyasema hayo wakati akihutubia umati wa wananchi mjini Arusha wakati wa mkutano wa kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa katiba ambapo amesema ukawa siku zote unapigania ukombozi wa taifa hili ili kuhakikisha wananchi wanapata katiba itakayotoa majibu ya kero za wananchi.
Naye mbunge wa jimbo la Moshi mjini Mh Philemon Ndesamburo amewahakikishia wananchi kuwa UKAWA utazunguka nchi nzima kuwaeleza wananchi ukweli juu katiba inayowasaidia kujikomboa katika umasikini.
Huko mkoani Iringa mamia ya wananchi wa wilaya ya Mufindi wamejitokeza kwa wingi katika mkutano wa UKAWA.
Akizungumza na wananchi hao mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF Prof Ibrahimu Lipumba amewataka wananchi wa Mufindi mkoani Iringa kuendelea kuunga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA ili watanzania wapate katiba itakayoweza kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi wenyewe na si kunufaisha wachache na kuwaacha wengine wakiendelea kuteseka kwa hali ngumu za maisha na kukosa huduma muhimu zikiwemo za afya na elimu.