Wednesday , 24th Jun , 2015

Zaidi ya wakazi elfu sita katika kitongoji cha Oltotoi Kijiji cha Narakawo wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wako hatarini kuambukizwa magonjwa ya milipuko na kuhara kutokana na ukosefu wa maji safi na salama.

Wananchi wa kata za Narakawo na Lobosiret zilizopo wilaya ya Simanjiro mkoa wa Manyara wakiwa mkutanoni.

Wakazi hao wamekiambia kituo hiki kwamba tatizo la ukosefu wa maji ni kubwa na limekuwa likiwalazimu wakinamama kutembea umbali wa kilomita zaidi ya thelathini kutafuta maji kitendo kinachoathiri shughuli za uzalishaji na kurudisha uchumi wao nyuma.

Mtendaji wa kijiji hicho Meshaki Tureto amesema kuwa tatizo la ukosefu wa maji linazidi kuongezeka kutokana na bwawa walilokuwa wanalitegemea kubomoka pamoja na visima vya muda kukauka, hivyo wanalazimika kufuata maji vijiji vya jirani kwa ajili ya kunyweshea mifugo zaidi ya elfu ishirini.

Changamoto hiyo imewasukuma wananchi kufanya zoezi la kuchangisha fedha kwa ajili ya kujenga matenki ya kuhifadhia maji.

Katika zoezi hilo mmoja wa wadau wa maendeleo katika eneo hilo Lenganasi Mdele, amewahimiza mwananchi kujitolea kwa hali na mali kutatua matatizo huku akiwakemea baadhi ya viongozi wanaowagawa wananchi kwa itikadi ya vyama jambo ambalo linaleta mgawanyiko mkubwa na kurudisha maendeleo nyuma.

Pamoja na Wilaya ya Simanjiro kuwa na rasilimali nyingi kama hifadhi za wanyama, idadi kubwa ya mifugo na ardhi kubwa yenye rutuba ikiwamo madini ya Tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee bado eneo hilo limekuwa na matatizo makubwa ya maji pamoja na ukosefu wa miundombinu suala linawafanya wakazi wa wilaya hii kuendelea kuwa masikini.