Thursday , 30th Jun , 2016

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji nchini imesema itaanzisha vituo maalum vya kuuzia na kukagua mazao ili kuhakikisha wakulima hawauzi mazao yaliyofungashwa kinyume na sheria ikiwa ni pamoja na lumbesa kinyume cha Sheria ya Wakala wa Vipimo.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage

Akijibu Maswali ya Wabunge Mjini Dodoma, katika kipindi cha maswali na majibu,Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Charles Mwijage amesema kila wilaya ianzishe mitaa ya viwanda ili kuwasaidia wakulima kunufaika na mazao yao kwa kudhibiti udanganyifu unaofanywa na wafanyabiashara kwa kuwanyonya wakulima.

Mhe. Mwijage amesema kuwa atalazimika kununua mizani pamoja na mashine za EFDS na kuweka vituo vya mauzo hayo ili kuleta tija kwa wakulima huku akiongeza kwa kusema kuwa sasa kutakuwa na kipimo maalumu cha uzito wa kufunga mizigo yao.

Kwa upande mwingine,akizungumzia viwanda vilivyobinafsishwa, Mhe.Mwijage amesema wawekezaji wote waliopewa viwanda na wameshindwa kuviendeleza serikali inawataka wavirudishe mara moja.