Friday , 11th Mar , 2016

Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kupambana na watumishi wa Umma wasiokuwa na maadili na uadilifu kazini lengo likiwa ni kushughulikia malalamiko yanayojitokeza kwenye wizara wakati wa kuajiri huku suala la udini na ukabila likitajwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki

Hayo yamebanishwa na Waziri wa nchi ofisi ya rais utumishi na utawala bora Mhe. Angela Kairuki wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya maadili kwa viongozi wa Umma kwa makatibu wakuu na manaibu wao kutoka wizara mbalimbali.

Bi. Angela amesema kuwa viongozi hao wanatakiwa kuweka mbele maadili ya utumishi na sio maslahi binafsi ili kuepuka lawama kwa watu wanao wahudumia ambao ni wananchi wa hali ya chini.

Mhe. Kairuki ameongeza kuwa kuna baadhi ya taasisi zimebainika kutoa ajira kwa ukabila hivyo amewataka viongozi hao kuwa makini katika suala hilo na kusema kuwa serikali yake itaendelea kusimamia hilo kuhakikisha mtu anaepata ajira anatokana na sifa stahiki.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Mhandisi John Kijazi amewatoa hofu watumishi wa umma juu ya umiliki wa mali huku akisisitiza kuwa zinapaswa kupatikana kisheria na kusema kuwa kama sheria zinamapungufu zinapaswa kurekebishwa.