Wednesday , 22nd Jun , 2016

Tukio la kihistoria la kupatwa kwa jua kipete linatarajiwa kutokea nchini Tanzania mnamo tarehe 1 Septemba mwaka huu majira ya saa nne asubuhi mpaka saa nane mchana.

Akitoa taarifa hiyo Mhadhiri wa fizikia na mtaalamu wa Sonomia katika kitivo cha sayansi chuo kikuu huria cha Tanzania Dkt Noorali Jiwaji amesema kuwa kwa mara ya mwisho tukio kama hilo lilitokea nchini Tanzania mwaka 1977 na linatarajiwa tena kutokea mwaka 2031.

Wataalam wamelichagua eneo la Lujewa mkoani Mbeya kuwa ndilo enelo ambalo watu wataweza kuona vizuri jua likiwa katika muundo wa pete kutokana na mwezi kukaa katikati yake majira ya saa nne na dakika 17 asubuhi.

Dkt Jiwaji ametoa wito kwa wanafunzi kuweza kufika eneo hilo kwa ajili ya kujionea yale waliokuwa wakiyasoma kwenye jiografia yakitokea kwa uhalisia , pia itakuwa kama ni sehemu ya kivutio kushuhudia jua likiwa linabadilika katika maumbo mbalimbali.

Aidha Dkt Jiwaji ametahadharisha juu ya watu kuangalia tukio hilo bila ya kuvaa vifaa maalum vya kuzuia mionzi ya jua kwani ni hatari kwa afya ya macho, vifaa pekee vinavyoshauriwa kutazamia jua ni miwani maalum yenye uwezo wa kuchuja nguvu ya jua kwa asilimia 99.999.