Thursday , 26th Mar , 2015

Serikali imeutaka mtandao wa mawasiliano ya simu za mkononi Tanzania TTCL kuboresha huduma zake hasa katika maeneo ya vijijini ambako mitandao mingine ya simu haifiki ili wananchi walioko pembezoni waweze kupata huduma bora za mawasiliano.

Wito huo umetolewa leo na Katibu tawala wa mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge kwenye uzinduzi wa mnara wa mawasiliano wa simu ya TTCL katika kata ya Nondwa iliyoko Wilayani Bahi Mkoani Dodoma.

Amesema ni lazima mtandao wa TTCL ujitanue na kuboresha huduma zake kwa wananchi kwa kuwa ndiyo mtandao pekee wa serikali wa simu za mkononi ambao unawafikia watu walioko vijijini.

Kwa upande wake Meneja wa TTCL mkoa wa Dodoma, Mhandisi Ekael Manase amesema kuwa mnara huo wa mawasiliano ya simu ya TTCL uliojengwa katika kata ya Nondwa ni kati ya minara 20 ambayo iko kwenye mradi wa serikali wa kupeleka mawasiliano katika kata 20 nchini ambazo hazina mawasiliano ya simu kabisa.