Monday , 3rd Oct , 2016

Shirika la Simu nchini (TTCL) limesema limejipanga kikamilifu kuhimili ushindani wa kibiashara uliopo kwenye soko la huduma ya mawasiliano nchini.

Limesema linaingia katika ushindani hasa baada ya serikali kurejesha hisa zake zote zilizokuwa zinamilikiwa na mbia mwenza na hivyo kulifanya shirika hilo kumilikiwa moja kwa moja na wananchi.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Bw. Waziri Waziri Kindamba, amesema hayo leo wakati shirika hilo likianza maadhimisho ya wiki moja ya huduma kwa wateja ambapo wafanyakazi na maafisa wa shirika hilo watakuwa wakisilikiliza mahitaji mbalimbali ya wateja, mahitaji ambayo utekelezaji wake utaleta mageuzi na ufanisi wa shirika hilo.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ambaye ameziagiza taasisi zote za umma zilizo chini ya ofisi yake kutumia huduma za mawasiliano zinazotolea na kampuni ya simu nchini kama njia ya kuchochea wigo wa mapato ya shirika hilo.