Wednesday , 15th Jun , 2016

Bodi ya Utalii nchini TTB imeanzisha mfumo maalumu ambao wafanyabiashara na watoa huduma za utalii wakiwemo wamiliki wa hoteli na nyumba za kulala wageni, wanaweza kutangaza biashara zao na hivyo kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii.

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa TTB Bw. Philip Chitaunga

Mfumo huo unapatikana kwa njia ya mtandao wa intaneti, ambapo watoa huduma za utalii wanaweza kuwafikia wateja wao hadi kwenye masoko ya kimataifa bila kujali wapo eneo gani la nchi kama anavyoeleza Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa TTB Bw. Philip Chitaunga.

"Mfumo huu unapatikana kupitia tovuti maalum ambapo vivutio vyote vya utalii nchini vinapatikana humo sambamba na kuwapa fursa watoa huduma za utalii kutangaza biashara zao pasipo gharama yoyote na hivyo kufikia wateja hadi kwenye masoko ya kimataifa," amesema Bw. Chitaunga.

Bw. Chitaunga amesema kuanzishwa kwa mfumo huo ni moja ya inayotumiwa na Bodi ya Utalii ya kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea Tanzania kutoka idadi ya sasa ya watalii milioni moja na laki moja hadi watalii milioni mbili kwa mwaka.

"Tofauti na aina nyingine za tovuti za utalii, mfumo huu mpya unamwezesha mtalii kupata taarifa za hoteli, usariri na nyumba za kulala wageni zilizopo hadi maeneo ya vijijini na ambazo wamiliki wake hawawezi kuzitangaza katika masoko hayo, huku suala jipya likiwa ni namna mteja anavyoweza kufanya malipo moja kwa moja kwa njia ya mtandao," amefafanua Kaimu Mkurugenzi huyo wa Masoko wa Bodi ya Utalii.