Friday , 20th Jan , 2017

Hatimaye Donald Trump kutoka chama cha Republican ameapishwa kuwa Rais wa 45 wa Taifa la Marekani akimrithi Barack Obama kutoka chama cha Democratic ambaye muhula wake umemalizika rasmi leo.

Donald Trum akila kiapo

Akihutubia maelfu ya wananchi waliokusanyika katika makao makuu ya Bunge la Congress ya Capital Building katika jiji la Washington DC, Rais Trump amesema muda wa kuongea  maneno matupu bila vitendo nchini humo umekwisha, na sasa ni kazi tu ili kurejesha utajiri wa taifa hilo uliopotea..

Amesema maamuzi yoyote yatakayofanyika yatatoa kipaumbele kwa Marekani kwanza, ikiwa ni pamoja na sera za nje, huduma za afya, elimu, na miundombinu na kwamba muda wa wanasiasa wasiotekeleza ahadi zao kwa vitendo umekwisha.

Katika hotuba iliyochukua kati ya dakika 10- hadi 15 amesema kuapishwa kwake kunamaanisha kukabidhi madaraka kwa umma wa Wamarekani.

Amesema, haijalishi ni chama gani kilichopo madarakani bali kikubwa ni kwa wananchi wa Marekani kuiongoza serikali yao na kwamba siku hii ya leo ni ya kwao.

Pia amesema kuwa atafanya kazi ya kuliunganisha taifa hilo bila ubaguzi wowote ili kuhakikisha heshima ya Marekani inarudi.

"Bila kujali rangi zetu, kwa pamoja tutaurejesha ukuu na utajiri wa Marekani"  Amesema Trump