Thursday , 7th Apr , 2016

Taasisi ya sekta binafsi nchini - TPSF imesema kamwe umaskini Tanzania sio mahala pake kutokana na fursa nyingi za kiuchumi ambazo nchi inazo hususani kwenye sekta ya kilimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF Dkt Godfrey Simbeye

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF Dkt Godfrey Simbeye amesema hayo leo na kutaja moja ya fursa za wazi kuwa ni katika zao la muhogo, ambalo amelitaja kuwa moja ya malighafi chache za kilimo inayohitajika na aina nyingi za viwanda lakini Watanzania hawajalichangamkia kulima kwa wingi na kuuza kama malighafi.

Dkt Simbeye amesema iwapo Watanzania watazitumia ipasavyo fursa zilizopo kwenye zao hilo, wanaweza kubadilisha kabisa uchumi wa nchi na kuboresha hali ya kipato chao na hivyo kufikia malengo ya dira ya taifa ya mwaka 2025 ya kuwa taifa lenye uchumi wa kati.

Dkt Simbeye ametaja baadhi ya matumizi ya muhogo kuwa ni katika utengenezaji wa wanga unaotumika kwenye viwanda vya pombe, huku sehemu nyingine ya wanga huo ikitumika katika viwanda vya nguo, vyakula kama biskuti huku majani yake yakitumika kama mbolea na chakula cha mifugo.