Friday , 20th Feb , 2015

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein ameitaka serikali ya Tanzania kuchunguza haraka na kuwafikisha mbele ya sheria watuhumiwa wa mauaji ya walemavu wa ngozi, Albino.

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein

Kauli hiyo ya Kamishna Zeid ameitoa kufuatia taarifa za kutekwa nyara kwa mtoto huyo mwenye umri wa mwaka mmoja na hatimaye maiti yake kupatikana ilhali baadhi ya viungo vyake vimenyofolewa.

Amelaani vikali kitendo hicho cha tarehe 17 Februari akisema mashambulizi yoyote dhidi ya Albino ambayo mara nyingi huchochewa na imani za kishirikina ni kinyume cha haki za binadamu.

Kamishna Zeid pia ametaka ulinzi uimarishwe dhidi ya raia hao hususan wakati huu ambapo nchi hiyo inaelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Tom Bahame Nyanduga ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora nchini Tanzania, ametoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kuelekea wapelelezi kanda ya Ziwa kwa ajili ya uchunguzi wa matukio hayo.

Hata hivyo amesema ni muhimu kuelimisha jamii ili kutokomeza unyanyapaa na fikra potofu juu ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Tangu mwaka 2000 watu 75 wenye ulemavu wa ngozi nchini Tanzania wameuawa.