Takwimu zilizotolewa na shirika la kulinda watoto la Save The Children katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika iliyofanyika jijini Dar es salaam, inaonyesha kuwa Asilimia 37 ya watoto wa kike nchini wameolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18, huku asilimia 22 wenye umri wa miaka 15 hadi 19 wamebebeshwa mimba.
Afisa elimu na usalama kwa watoto kutoka save the children bi Haika Harrison amesema ndoa za utotoni zimekuwa na matokeo mabaya katika jamii ikiwemo, kumnyima haki ya elimu, maambukizi ya virusi vya ukimwi, matatizo ya uzazi na vifo, ukatili wa kijinsia pamoja na kuminya fursa za kiuchumi.
Naye Afisa mtendaji mkuu wa kituo cha huduma ya simu kwa mtoto Kiiya Joel Kiiya amesema zaidi ya asilimia 70 ya taarifa za ukatili wa kingoni kwa watoto zinazoripotiwa katika kituo hicho azichukuliwi hatua jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada za kupambana na ukatili kwa watoto.
Joel Kiiya amesema kwa mwezi moja wanapokea taarifa hadi 28 jambo linaloonyesha ukubwa wa tatizo la ukatili kwa watoto nchini huku Wilaya ya Temeke mkoa wa Dar es salaam ndio unaoongoza kwa kuripoti ukatili wa kingono kwa watoto
Mmoja wa Watoto walioojiwa na East Africa Radio kuusiana na uelewa wao juu ya siku hii, Anna Sembani amesema wanategemea wazazi watawalinda dhidi ya ukatili wowote sambamba na kuwapa fursa ya elimu kwa jinsia zote kwani ulinzi imara dhidi yao ndio ujenzi wa taifa la kesho.