
Akiongea na East Africa Radio Mwanasheria wa Kituo cha Usuluhishi TAMWA, Bi. Suzan Charles amesema uzoefu wao katika kusuluhisha kesi wamegundua kuwa baadhi ya wanandoa hawajui sheria hizo.
Aidha Bi. Suzan amesema kuwa TAMWA inapendekeza serikali katika mchakato wake wa kubadilisha sheria ya ndoa iweke kipengele kitakachowataka wanandoa watarajiwa kupata elimu ya ndoa na sheria zake kabla ya kuingia kwenye ndoa ili kusaidia kumaliza tatizo la migogoro ya ndoa ambayo inaonekana kukithiri katika jamii.
Katika hatua nyingine Bi. Suzan ameshauri kuwepo na maboresho ya matangazo ya ndoa hasa kwa wale wanaoamini katika ndoa moja pekee kwani baadhi ya wanandoa wamekuwa sio waaminifu na kuamua kufunga ndoa zaidi ya moja hali inayowawia vigumu TAMWA kutatua migogoro ya watu wanaokuja na vyeti halali vya ndoa kwa mume mmoja bila ya wao kujua.