
Mh. Joseph Mbilinyi kushoto na Spika Job Ndugai kulia.
Mh. Mbilinyi aliuliza swali hilo wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, ambapo alihoji kwanini bunge lisichukue hatua ya kusaidia wananchi wa Mbeya ambao wameporwa mali zao na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Baada ya Sugu kumaliza kuuliza Spika hakuruhusu Waziri mwenye dhamana ya Habari Dkt. Harrsion Mwakyembe kujibu badala yake alisema alichoongea Mh. Mbilinyi sio kweli hivyo akafuta swali hilo.
''Swali lako halihusiani kabisa na swali la msingi la Mh. Devotha Minja na wala sio la wizara ya habari na kwa vile ulichoongea sio kweli swali hilo nalifuta'', alisema Ndugai.
Awali kabla ya Sugu kuuliza swali hilo ambalo lilikuwa la nyongeza, lilitanguliwa na swali la msingi la mbunge wa Viti maalum Devotha Minja, ambalo lilihoji kwanini serikali isivichukue viwanja vya michezo vinavyomilikiwa na CCM ili kuviendeleza kutokana na miundombinu yake kuchakaa.
CCM inamiliki asilimia kubwa ya viwanja nchini kwa mfano CCM Kirumba Mwanza, CCM Kambarage Shinyanga, Sheikh Abeid Karume Arusha, Ali Hassan Mwinyi Tabora, CCM Mkwakwani Tanga na vingine vingi.