Monday , 23rd Mar , 2015

Waziri wa Uchukuzi Mhe.

Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, mhe. Samuel Sitta.

Waziri wa Uchukuzi Mhe. Samuel Sitta, amesema hatokubali kuona viwanja vya ndege nchini vinakuwa uchochoro wa kupitishia dawa za kulevya na kwamba atahakikisha usafirishaji wa dawa hizo nchini unakomeshwa kabisa.

Akizungumza katika mahojiano na East Africa Radio muda mfupi baada ya kuongelea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya hali ya hewa, Waziri Sitta amesema hivi sasa wasafirishaji wa dawa hizo wamebadili mbinu na kuanza kutumia njia ya bahari baada ya ulinzi kuimarishwa katika viwanja vya ndege na katika maeneo ya mipakani.

Waziri Sitta amewataka vijana nchini kuacha tamaa ya kupata pesa na utajiri wa haraka haraka kwa kutumiwa kuuza na kusafirisha dawa za kulevya kwani kitendo hicho kinayaweka maisha yao hatarini na kufifisha ndoto za kufanikiwa kimaisha kwa kufanya kazi na shughuli zilizo halali.

Katika hatua nyingine, waziri Sitta amesema mamlaka zinazosimamia usafiri wa anga na sekta ya utalii katika nchi za Tanzania na Kenya, zimeanza kutekeleza makubaliano ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na mwenzake Uhuru Kenyatta, ya kuondoa vikwazo vyote vilivyowekwa kwenye sekta hizo baada ya kuwepo kwa mvutano baina ya nchi hizo mbili.

Vikwazo hivyo ni pamoja na hatua ya serikali ya Kenya kuzuia magari yaliyobeba watalii yasiingie katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, hatua ambayo iliilazimu serikali ya Tanzania nayo kupunguza safari za ndege za shirika la ndege la Kenya KQ kutoka safari 52 kwa wiki hadi safari 14 kwa mujibu wa mkataba wa ushirikiano katika sekta ya utalii wa mwaka 1985.

Mhe. Samuel Sitta amesema sababu zilizopelekea mvutano huo ni fundisho juu ya umuhimu wa kuwepo kwa mazungumzo baina ya nchi jirani hususani kwa masuala nyeti yanayogusa ushirikiano baina ya nchi hizo.