Monday , 26th Jan , 2015

Waziri wa Nishati na Madini nchini Tanzania George Simbachawene ameahidi kukuza na kuboresha upatikanaji wa umeme Vijijini kwa kurekebisha sera ya gesi ili kusaidia uzalishaji.

Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene

Akiongea hii leo Jijini Dar es Salaam wakati wa makabidhiano ya ofisi, Simbachawene amesema mradi wa gesi utakapokamilika utasaidia kuzalisha umeme wa gharama nafuu utakaosambazwa katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo.

Simbachawene amesema kuwa nchi ya Tanzania imefanikiwa kupata kiwango kikubwa cha gesi na kuwa watahakikisha gesi hiyo inaawanufaisha wananchi na kueleza upatikanaji wa umeme wa bei nafuu utasaidia kuboresha maisha ya wanainchi.

Simbachawene amewataka wachimbaji wadogo kutumia fursa zilizopo na kukubali ushindani uliopo na kuachana na kulalamika kuwa hawapewi nafasi katika uwekezaji.

Akiongea leo jijini Dar es Salaam wakati akieleza vipaumbele vyake baada ya kukabidhiwa ofisi waziri Simbachawene amesema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wachimbaji wadogo wakidai kunyimwa fursa za uwekezaji na kuwataka kuungana ili waweze kukusanya mitaji yenye kuwawezesha kununua mitambo ya kisasa yenye kuendana na ushindani na mabadiliko ya tekinolojia.

Aidha Simbachawene ameongeza kuwa wizara yake itashirikiana na EWURA ili kuweza kuweka utaratibu wa marekebisho katika bei za mafuta ziendane na soko la Dunia

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania Mh. Angela Kairuki amesema hayupo tayari kufanya kazi na watendaji wa wizara hiyo ambao watabainika kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi na kushiriki katika vitendo vya rushwa.

Akizungumza na watendaji wakuu wa wizara hiyo leo, Mh. Kairuki ambaye aliongozana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wiliam Lukuvi amesema migogoro ya ardhi sasa inahitajika kumalizwa kwa ushirikiano kati ya wananchi wa eneo husika, kwani imebainika migogoro hiyo imekuwa ikichangiwa na baadhi ya watendaji wizarani hapo.

Mh Kairuki amepiga marufuku urasimu uliokuwepo kwa muda mrefu kwa wananchi kucheleweshwa kupata hati za viwanja pasipo na sababu za msingi.