Saturday , 2nd May , 2015

Idara ya uvuvi mkoani Kagera imeteketeza kwa moto shehena ya zana haramu za uvuvi zenye thamani ya zaidi ya shilimgi milioni 200 zilizokuwa zikitumika kuangamiza samaki wachanga katika ziwa Victoria.

Afisa mfawidhi wa uvuvi mkoa wa Kagera Apolinary Kyojo akiwa katika tukio la uteketezaji wa zana hizo.

Akizungumza mara baada ya kutekeza kwa moto zana haramu za uvuvi zikiwemo nyavu za macho madogo na makokolo afisa mfawidhi wa uvuvi mkoa wa Kagera Apolinary Kyojo amesema zana hizo zilikamatwa wakati wa operesheni ya linda ziwa Victoria iliyofanyika hivi karibuni kwa siku kumi na nne.

Kwa upande wake afisa mfawidhi wa uvuvi mkoa wa Geita Deogratius Pande amesema kuwa zoezi la kufanya doria katika ziwa hilo ni endelevu na kuwataka wavuvi kufuata kanuni na sheria za uvuvi

Mapema akiongea katika tukio hilo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kagera John Mongera kaimu katibu tawala wa mkoa wa Kagera Renatus Bamporiki ameitaka idara ya uvuvi kujikita zaidi katika kufanya doria za kushitukiza na kuwabaini wavuvi wanaotumia zana haramu.

Aidha Bamporiki amevitupia lawama vikundi vya kulinda rasilimali za uvuvi katika ziwa Victoria bmu kushindwa kusimamia kikamilifu na kutoa taarifa juu ya wavuvi haramu.

Kwa upande wake mtaalamu wa udhibiti na doria kutoka nchini Afrika Kusini Andrias Freez ameitaka serikali ya Tanzania kupitia wizara ya uvuvi na maendeleo ya mifugo kujikita zaidi katika kulinda ziwa Victoria na kufanya operesheni za kisayansi zinazokwenda sambamba na kutoa elimu kwa wavuvi na siyo kutumia nguvu kubwa kuwakamata wavuvi na kuwasurubisha bali itoe elimu kwa wavuvi ili wasijihusishe na uvuvi haramu kwa manufaa ya kizazi hiki na kijacho.

Ikumbukwe kwamba Operesheni Linda Ziwa Victoria ilikuwa ya kisayansi na imefanyika katika mikoa ya Kagera na Geita kwa kushirikiana na jeshi la polisi pamoja walifanikiwa kukamata shehena ya zana haramu na hatimaye leo zimeteketezwa kwa moto.