Kamati ya Msaada wa Kisheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa madai ya kuhusika katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Kesi hiyo iliyofunguliwa kwa kushirikiana na Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, inahusu ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na serikali kupitia kwa aliyekuwa waziri wa afya Dkt Aron Chiduo, ambaye aliruhusu kufanyika kwa majaribio ya chanjo ya ugonjwa wa UKIMWI kinyume na taratibu.
Msingi wa kesi hiyo unatokana na madhara waliyoyapata watu waliotumika katika majaribio ya chanjo hiyo ijulikanayo kama Virodene P058 iliyotengenezwa na kuletwa nchini na kampuni ya Virodene Pharmaceutical PTY ya nchini Afrika Kusini.
Chanjo hiyo inadaiwa kuleta madhara mbalimbali ya kiafya kwa waliofanyiwa majaribio hayo ambapo kati ya watu zaidi ya Sitini waliofanyiwa majaribio, wengi wamepoteza maisha na hivi sasa wamebaki watu saba tu ambao nao wanalalamika kupatwa na madhara mbalimbali ikiwemo kudhohofika kusiko kwa kawaida kwa afya zao.
Waathirika wa chanjo hiyo ambao kimsingi ndio walalamikaji wakuu ni Bw. Steven William Kimaro, Bahari Sefu, Juto Ramadhani, Ahmed Said Mwiru, Dickson Masena, Octavunus Francis Dupya na Mhando Haji Majuwe.
Kwa mujibu wa wakili anayewatetea walalamikaji hao ambaye pia ni mhadhiri wa sheria wa chuo kikuu cha Dar es Salaam mwalimu James Jesse; serikali imeingia matatani kutokana na waziri aliyepewa dhamana ya afya kati ya mwaka 1999 na 2002 Dkt Aron Chiduo, kuruhusu kufanyika kwa majaribio ya chanjo hiyo licha ya taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu NIMR kukataa isifanyike nchini kutokana na kutokidhi viwango vya kujaribiwa kwa binadamu.
Wakili Jesse amesema, Dkt Chiduo alitumia vibaya madaraka yake kwa kutofuata maamuzi yaliyochukuliwa na NIMR ambapo inadaiwa kuwa kwa kutumia mamlaka yake kama waziri wa afya, aliruhusu chanjo hiyo ifanyike katika hospitali kuu ya Jeshi Lugalo, na katika kituo cha afya cha Chadibwa ambacho amedai kuwa kilikuwa kinamilikiwa na aliyewahi kuwa mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Omar Mahita.
HISTORIA YA VIRODENE NCHINI TANZANIA
Dawa ya Virodene ni chanjo inayosemekana kuwa na uwezo wa kutibu UKIMWI iliyogunduliwa mwaka 1995 huko Afrika Kusini na wanasayansi Bw. na Bi. Michelle Visser.
Dawa hii ilijaribiwa kwa wagonjwa kumi na moja huko Afrika Kusini. Baadaye dawa hiyo ilipigwa marufuku nchini humo baada ya kugundulika kuwa na kemikali sumu ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu. Jaribio la wanasayansi hao kutaka kufanya utafiti wa Virodene nchini Ujerumani na Uingereza zilishindikana baada ya kunyimwa vibali.