
Serikali ya Tanzania imeombwa kufuta ushuru wa kuingiza nchini bidhaa mbalimbali za kuwasaidia watu wenye ulemavu ngozi (albinism).
Shirika la kimataifa linalowahudumia watu wenye ulemavu wa ngozi la Under The Same Sun (UTSS) limetoa wito huo wakati likipokea vifaa mbalimbali vya kuwasaidia watu wenye albinism kutoka kwa watu wa Korea kwa ushirikiano na shirika la United Help For International Children lililopo mjini Tanga.
Afisa Uendeshaji wa shirika hilo Gamariel Mboya amevitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni losheni na miwani maalumu ya kuzuia mionzi ya jua, hatua aliyosema inafaa iende sambamba na kuondoa vikwazo kwa wahisani wanaowahudumia albino kama moja ya njia za kuwasaidia watu wenye albinism nchini.