Friday , 7th Nov , 2014

Tanzania imeshtushwa na ripoti inayoelezea biashara haramu ya meno ya tembo kati ya baadhi ya viongozi wa nchi hiyo na China

Shehena ya Pembe za Ndovu

Serikali ya nchi hiyo imesema imesikitishwa na ripoti iliyotolewa na taasisi ya uchunguzi ya mazingira inayodai kwamba majangili wa kichina wakishirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali ya Tanzania ndio wanaoangamiza idadi ya tembo kutokana na biashara haramu ya meno ya tembo.

Inadaiwa kwamba raia wa China walitumia ziara ya rais wao nchini humo kusafirisha kimagendo maelfu ya kilo za pembe za ndovu.

Kulingana na shirika la utafiti wa mazingira, EIA, Pembe hizo zilinunuliwa wiki moja tu kabla ya ziara ya rais huyo nchini tanzania mwaka jana na zilifichwa katika mifuko ya wanadiplomasia ili zisitambuliwe.

Msemaji wa serikali Assah Mwambene amesema ripoti kama hiyo inatatiza jitihada za serikali kukabiliana na uuzaji haramu wa pembe za ndovu.