Wednesday , 14th Jan , 2015

NAIBU Waziri wa Maji Amos Makalla amesema kuwa serikali inatarajia kupeleka maji katika vijiji vyote ambavyo vipo katika vyanzo vya maji na havina huduma hiyo hapa nchini kwa lengo la kuhamasika kuendelea kulinda vyanzo hivyo.

Naibu waziri wa Maji Mhe Amos Makalla akikwepa utelezi wakati akikagua chanzo cha maji ya chemchemu ya Ndoba kijiji cha Galijembe

Makalla ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika kijiji na kata ya Kifume halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe alisema kuwa vijiji ambako vyanzo vya maji ya kata ya Kifume, Serikali itahakikisha wananchi watapatiwa maji.

Amesema kuwa Wizara ya Maji ina mpango wa kuhakikisha vijiji vyote hapa nchini vinapatiwa maji ili kuimarisha ulinzi wa vyanzo hivyo vya maji na kuwa miradi hiyo kuwa ya kudumu.

Awali akizungumza katika mkutano wa hadhara mbunge jimbo la Njombe Kaskazini, Deo Sanga amesema kuwa tangu nchi ipate uhuru vijiji vya kata ya Kifume havijawahi kupata maji na sasa mwaka huu wananchi hao wanafurahia kupata maji, na kuachana na shughuri za kuhangaikia maji na kufanya shughuli za kimaendeleo.