Friday , 24th Jul , 2015

Serikali imeanza utaratibu wa kuanza kudhibiti kingo za bahari hindi zinazopakana na makazi ya watu katika maeneo mbali mbali nchini ikiwemo wilaya ya pangani ili kuepuka maafa yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi.

Waziri wa nchi,Ofisi ya makamu wa Rais mazingira Dkt. Binilith Mahenge

Akizungumza wilayani Pangani kuhusu jitihada za serikali za kudhibiti majanga kwa wakazi wanaoishi pembeni mwa kingo za bahari, Waziri wa nchi Ofisi ya makamu wa Rais mazingira Dkt. Binilith Mahenge amesema zaidi ya dola za kimarekeni mil 4 zimetolewa na mfuko wa kimataifa unaoshughulikia mazingira kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo hapa nchini.

Akifafanua zaidi Dkt. Mahenge amesema maeneo ambayo yatafikiwa na mradi huo unaotarajiwa kuanza kabla ya uchaguzi mkuu ni kingo za bahari zilizopo wilayani Pangani, Ocean Road, Chuo cha Mwalimu Nyerere kilichopo kivukoni, Zanzibar pamoja na kupanda mikoko katika maeneo hayo kwa ajili ya kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema hatua hiyo inatokana na serikali kusaini mkataba na mkandarasi shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia utoaji wa huduma za maafa zikiwemo za mabadiliko ya tabia nchi ambapo tayari limekwishafanya upembuzi yakinifu na kilichobakia ni serikali kumtafuta mkandarasi ili aweze kuanza zoezi hilo la ujenzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.