Thursday , 13th Mar , 2014

Serikali ya Tanzania, imeombwa kuwapa semina za jinsi ya uendeshaji wa shughuli za bunge, wabunge 201 walioteuliwa na rais kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii ambao wanaunda bunge maalumu la katiba.

Akizungumza na East Africa Radio kwa njia ya simu kutoka mjini Dodoma, mmoja wa wajumbe wa bunge la katiba ambaye ni katibu mkuu wa chama cha wakulima AFP Rashid Ra,i amesema kuwa kuna umuhimu wabunge hao kupata semina ya jinsi ya kuendesha shughuli za bunge ili waweze kuwasilisha mawazo yao ipasavyo.

Rai amesema kuwa baadhi ya wabunge hao wanashindwa kuwasilisha masuala mbalimbali na wamekuwa wakiwasha maiki na kujibishana kama wapo sokoni, kutokana na kutofahamu kanuni na taratibu zinazosimamia uwasilishaji, kupinga na kutoa hoja.

Aidha amewataka wabunge kutoka katika vyama mbalimbali vya siasa kuacha ubinafsi kwa kutetea hoja za vyama vyao ambazo hazina manufaa kwa watanzania ambao matarajio yao ni kupata katiba ambayo itamkomboa na kumsaidia mtanzania katika masuala ya elimu, uchumi, afya, pamoja na miundombinu.