Rai hiyo imetolewa na Mwanazuoni Adam foya, alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Super mix kinachorushwa na East Africa Radio, kuhusu serikali ijayo itawatumia vipi vijana wasomi katika kukuza uchumi wa sekta mbali mbali.
Foya amesema vijana wote ambao wana elimu na wasio na elimu wana nafasi ya kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi, hivyo serikali ina wajibu wa kutoa mazingira ya vijana kushiriki katika shughuli mbali mbali za kiuchumi.
"Vijana wasomi na ambao hawakupata fursa ya kusoma, wote wana nafasi ya kuwa na mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi, lakini kinachopaswa kifanyike kikubwa zaidi ni kutoa mazingira ya vijana kushiriki katika shughuli mbali mbali za kiuchumi, either za kuajiriwa au za kujiajiri na zenye maslahi bora kwa hawa vijana, tukumbuke kwamba vijana ndio wenye nguvu, ni sehemu kubwa zaidi ya Taifa letu", alisema Foya.
Adam Foya amesema kwa sasa vijana wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosa elimu hususan ya vitendo, ambayo inawawezesha kujiajiri wenyewe na kuchangia uchumi wa Taifa pasipo kususbiri kuajiriwa.
" Changamoto mojawapo iliyopo kwa vijana katika kushiriki katika sekta mbali mbali kuna suala zima la elimu, elimu isiishie tu elimu ya nadharia bali iwe ni elimu ambayo ina uwezo wa kuwafanya vijana wanapomaliza ngazi fulani za masomo, wawe wana uwezo wa kushiriki katika shughuli mbali mbali za kiuchumi", alisema Foya.
Pia Adam Foya amesema kuna uhitaji wa kuwezesha upatikanaji wa mitaji hususan wa rasilimali watu na ushauri kwa vijana, katika kuanzisha shughuli za maendeleo na kuziendeleza ili ziweze kuinua uchumi wa Taifa.