Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiibu maswali bungeni
Akizungumza leo Bungeni Mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa tayari serikali imeshajua gharama zinazotumika kwa usafirishaji hivyo serikali itakua inapanga bei dira kadri gharama hizo zinavyopanda na kushuka.
Mhe. Majaliwa amesema serikali inafanya hivyo ili kuwalinda wananchi wa kawaida kununua bidhaa hiyo kwa bei ya juu na ndio maana serikali kupitia Bodi ya Sukari ikaagiza sukari ili kupuguza upungufu wa bidhaa hiyo sokoni.
Mhe. Majaliwa amesema serikali imejihakikisha kuwa uingizwaji wa sukari nchini uliofanywa hautaathiri uzalishaji wa viwanda vya ndani lakini pia tatizo hilo litakwisha mara baada ya viwanda vya sukari kuanza uzalishaji ifikapo mwezi Julai mwaka huu.
Waziri Mkuu amesema mahitaji ya sukari nchini mpaka sasa ni tani 420,000 lakini mpaka sasa viwanda nchini vinatengeneza sukari kwa tani 300,000 hivyo kuna upungufu wa tani 100,000 na ndio maana serikali ilichukua hatua ya kuagiza sukari kwa utaratibu maalumu.
Amesema kuwa endapo serikali ingetoa kibali cha watu kuingiza sukari basi ingeingia kwa wingi kiasi ambacho ingeweza kuathiri soko zima la uzalishaji wa sukari kwenye viwanda vya nchini Tanzania.