Aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt Jakaya Kikwete akionesha kitabu cha sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, katika tukio la uzinduzi wa sera hiyo jijini Dar es salaam, mwezi Feb. mwaka 2015.
Wahadhiri wa elimu ya juu nchini Tanzania wamesema sera ya elimu ya mwaka 2014 kutozungumzia namna ya kuboresha shule za umma pamoja na mazingira ya ufundishaji kutaendelea kuchangia elimu kutoendana na utawandawazi na wahitimu wengi kutokuwa na ujuzi wa kufanya kazi kwa vitendo.
Katika majadiliano ya pamoja baina ya wahadhiri wa vyuo vya elimu ya juu wakikutanishwa na shirika lisilo la kiserikali la Haki Elimu, Mwalimu mtafiti na mchambuzi wa sera Mtemi Zombwe amesema serikali iangalie upya ili kubaini ni kwa nini wanafunzi wa elimu ya msingi huhitimu darasa la saba wakiwa hawajui kusoma.
Wahadhiri kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam wanasema serikali ianze kutoa chakula katika shule za msingi ili wanafunzi wanaotoka katika kaya masikini waweze kuongeza kiwango cha kuelewa katika maeneo ya vijijini pamoja na kufanya tathimini ya kina juu ya mpango wa kutoa elimu ya bure pamoja na kuondokana na matabaka katika utoaji wa elimu.
Prof. Suleman Sumra amesema amekuwepo katika mfumo wa elimu kwa miaka 50, na anaona kwamba elimu ya sasa imeparanganyika kwa kiwango kikubwa .
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Haki Elimu John Kalage amesema utofauti wa ubora wa elimu kati ya shule za umma na za binafsi unapelekea wanafunzi wanaohitimu shule za umma kuwa na maarifa duni.
Amesema shirika lake limeanisha baadhi ya mapungufu yaliyomo kwenye sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ili yafanyiwe kazi huku akisisitiza kuwa endapo mambo hayo yatafanyiwa sera hiyo itakuwa bora kuliko ilivyo hivi sasa.