Wednesday , 8th Jun , 2016

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Manunuzi na Ugavi nchini Tanzania Bw. Clemence Tesha amewataka watumishi kuzingatia maadili.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Manunuzi na Ugavi nchini Tanzania Bw. Clemence Tesha amewataka watumishi kuzingatia maadili yale waliojifunza wakiwa mafunzoni ili waweze kufanya kazi kwa kuzingatia maadili.

Bw. Tesha ametoa kauli hiyo hii jana wakati akiongea na maafisa wanafunzi wa shule ya mafunzo ya huduma na utawala Pangani na wakufunzi walipoitembelea bodi hiyo kwa lengo la kujifunza kwa vitendo ambapo amebainisha kuwa changamoto kubwa inayosiumbua tasnia ya manunuzi na ugavi nchini ni ubora wa vitu vinavyonunuliwa.

Aidha Bw Tesha amesema kuwa hivi sasa dunia inabadilika kulingana na wakati hivyo mambo ambayo yalionekana kufaa ikwa kipindi fulani yanaweza kuwa hayafai kwa kipindi kilichopo sasa hivyo ni muhimu kuwepo mafunzo yatakayowafanya watumishi kuendana na mazingira husika.

Kwa upande wake Mkuu wa Kombania ya Mafunzo ya Maafisa wa Shule ya Huduma na Mafunzo ya Utawala Pangani Meja Mustapha Makumbi amesema kuwa ni wakati sasa wa serikali kuhakikisha kuwa na mafunzo ya vitendo ya mara kwa mara ili kuweza kuwapa uwezo watumishi waweze kuendana na maadili ya utumishi.