Tuesday , 20th Jan , 2015

WANAWAKE wa (CHADEMA), Arusha,wametakiwa kujitokeza kwa wingi, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi bila woga katika uchaguzi mkuu ujao na kuonywa kujiingiza katika kashfa za kutembea na viongozi wao ili wapate nafasi hizo.

Makamu Mwenyekiti Taifa wa Baraza la Wanawake Chadema ,Bi. Hawa Mwaifunga

Akizungumza jana na Baraza la Wanawake Chadema Mkoani Arusha (BAWACHA), Makamu Mwenyekiti Taifa wa Baraza hilo, Hawa Mwaifunga, amesema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wanawake kujiingiza katika vitendo vya mapenzi na viongozi wa chama, ili wapate nafasi za uongozi kwa wepesi, jambo ambalo katika uongozi wake hatakubaliana nalo.

Aidha amesema endapo mwanachama ataamua kutembea na kiongozi hayo ni mapenzi yake ila kitakachombeba ndani y chama ili awe kiongozi ni kazi atakayofanya.

Hawa ameonya wanawake kuacha majungu na kuwapiga vita wenzao wanaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali, badala yake wawaunge mkono ili waweze kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama.

Amesema masuala ya kubebana ndani ya chama kwa mwaka huu wa uchaguzi hayatakuwepo ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

Pia amewaomba wanawake kuhamasishana na kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura mara tu litakapoletwa na hata kama uandikishwaji utakuwa unasumbua wasikate tamaa wakomae mpaka wajiandikishe, hiyo ndiyo njia pekee ya kuwaondoa mafisadi katika utawala.

Katika hatua nyingine amewaagiza viongozi wa baraza la Wanawake Mkoa wa Arusha, kuhakikisha wanafuatilia viongozi wanne wa baraza hilo wa kila kata, ili kuona kama wanatekeleza majukumu yao na endapo watagundua wamelega lega wawaondoe na kuweka wengine wenye uwezo wa
kusukuma mbele baraza hilo.