Wednesday , 29th Jun , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa wakuu wa wilaya watatu ambao walikuwa miongoni mwa wakuu wa wilaya 139 walioteuliwa hivi karibuni.

Sehemu ya wakuu wa wilaya waliohudhuria hafla hiyo, leo Ikulu jijini Dar es salaam.

Maamuzi hayo yametangazwa leo katika ukumbi wa Ikuklu jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kuapisha wakuu wapya wa mikoa pamoja na kiapo cha uadilifu kwa wakuu wapya wa wilaya.

Katika mabadiliko hayo madogo Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mteule Mhe. Fatma Hassan Toufiq na badala yake amemteua Bi. Agness Elias Hokororo kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo.

Sababu za maamuzi hayo ni kutokana na kwamba Fatma Hassan Toufiq ni mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo asingependa awe na nyazifa mbili kwa wakati mmoja, na kwamba awali uteuzi wake ulifanyika kimakosa.

Pia, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mteule Bw. Fikiri Avias Said na badala yake amemteua Bw. Miraji Mtaturu kuwa Mkuu wa wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa Rais, uteuzi jina la Fikiri Avias Said liliwekwa kimakosa katika orodha ya ma Dc wapya, na kwamba hakuwa amekusudiwa yeye, na kwamba tayari mawasiliano yamefanyika na mtu aliyekusudiwa ambaye ni bw Mtaturu alikwisha taarifiwa na alikuwepo ukumbini kwa ajili ya kiapo hicho pamoja na maelekezo mengine.

Na katika mtindo uliowaacha wengi midomo wazi, ametengua uteuzi wa Mkuu wa wilaya ya Serengeti Mteule Bw. Emile Yotham Ntakamulenga na badala yake amemteua Bw. Nurdin Hassan Babu kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo.

Maamuzi ya kutengua uteuzi huo yametangazwa wakati tayari Bw. Emile Yonathan akiwa ukumbini dakika chache kabla ya kula kiapo cha uadilifu, ambapo Mwenyekiti wa Sekretariet ya Maadili ya Utumishi wa Umma Jaji Salome Kaganda alimtaka atoke nje ya ukumbi kwa kuwa uteuzi wake umetenguliwa, na hivyo hakustahili kuwemo ndani ya ukumbi huo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakuu wa wilaya wateule kwenda kuchapa kazi na kutatua kero za wananchi katika wilaya zao huku wakizingatia kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.