Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akihutubia wakati wa uzinduzi wa Mwaka Mpya wa Kimahakama katika viwanja vya Mahakama vya Mtaaa wa Chimala Ocean Road jijini Dar es salaam February 2, 2017
Mhe. Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 02 Februari, 2017 katika sherehe za uzinduzi wa mwaka wa Mahakama (Siku ya Sheria) zilizofanyika katika uwanja wa Mahakama uliopo Mtaa wa Chimala, Kivukoni Jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2016 Serikali haijalipwa kiasi cha Shilingi Trilioni 7.5 licha ya kushinda kesi za ukwepaji kodi zilizokuwa zinawakabili washitakiwa mbalimbali.
Dkt. Magufuli ameipongeza Mahakama na wadau wake kwa kazi kubwa inayofanywa kuleta mabadiliko na uboreshaji wa huduma na miundombinu na ametaka kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Umuhimu wa utoaji wa haki kwa wakati kuwezesha ukuaji wa uchumi” itekelezwe vizuri kwa kutanguliza maslai ya Taifa ikiwemo kuhakikisha wanaopatikana na hatia ya kukwepa kodi wanalipa.
“Haiwezekani mwekezaji anachimba madini yetu, kodi halipi, anashitakiwa mahakamani anashindwa, halafu pesa haitolewi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiongea na Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamisi Juma wakati wa uzinduzi wa Mwaka Mpya wa Kimahakama katika viwanja vya Mahakama vya Mtaaa wa Chimala Ocean Road jijini Dar es salaam February 2, 2017
“Sasa tujiulize, kama utoaji haki unaakisi ujenzi wa uchumi wa nchi ni kwa kiasi gani kesi zenye thamani ya Shilingi Trilioni 7.5 zimeathiri uchumi?” amehoji Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mahakama wajipange kwa pamoja ili kushughulikia ipasavyo mashauri mbalimbali na kuondokana na migongano ambayo imekuwa ikidhohofisha ufanisi wa shughuli za kimahakama.
Pia Dkt. Magufuli ameahidi kushughulikia tatizo la ufinyu wa bajeti na maslai ya wafanyakazi wa Mahakama wakiwemo Majaji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiagana na majaji wa Mahakama ya Rufaa na wa Mahakama kuu baada ya sherehe za uzinduzi wa Mwaka Mpya wa Kimahakama katika viwanja vya Mahakama vya Mtaaa wa Chimala Ocean Road jijini Dar es salaam February 2, 2017
Pamoja na kumpongeza na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwa Mahakama, Kaimu Jaji Mkuu wa Mahakama Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma amesema katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama, mwaka 2016 jumla ya mashauri 279,331 yamesikilizwa sawa na asilimia 101 ya matarajio ya kusikiliza mashauri 276,147, Mahakama imefanikiwa kumaliza kesi 248 kati ya kesi 249 za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zilizohusisha Ubunge na Udiwani na pia Mahakama Kuu imefanikiwa kuanzisha Divisheni ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi (Mahakama ya Mafisadi)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akikabidhi kwa Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai ripoti ya mahakama kuhusu kesi za uchaguzi wakati wa uzinduzi wa Mwaka Mpya wa Kimahakama katika viwanja vya Mahakama vya Mtaaa wa Chimala Ocean Road jijini Dar es salaam February 2, 2017
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. John Kijazi, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand Leons Wambali, Majaji wa Mahakama Kuu, Mawakili, Viongozi wa Dini na Siasa na wawakilishi wa Taasisi mbalimbali.