Umati uliohudhuria mkutano wa CHADEMA Nzega
Jeshi la polisi limetahadharishwa kuacha tabia ya kutumia nguvu kupita kiasi linapokabiliana na matukio mbalimbali ikiwemo mikutano ya wanasiasa na maandamano ya wananchi hali ambayo inachangia baadhi ya wananchi kuuawa na wengine kusababishiwa ulemavu wa kudumu pasipo sababu na hivyo kulichukia.
Tahadhari hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar Salum Mwalimu na mbunge wa jimbo la Arusha mjini Godbless Lema wakati wakihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Nzega kwenye mkutano ulioandaliwa kwa ajili ya kumbukumbu ya siku thelathini za kuuawa kwa mmoja wa wanachama wa chama hicho Batholomeo Edward kwa kupigwa risasi na askari wa jeshi la polisi wakati wakisubiri matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
Naye mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Tabora Francis Msuka amelaani vikali tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali wilayani Nzega kwenda hospitali ya wilaya hiyo kumsalimia na kuanza kumdhihaki majeruhi Lucas Daudi ambaye pia aliyejeruhiwa mkono na mbavu za kushoto kwa kupigwa risasi na askari hao wa polisi.
Batholomeo Edward alifariki dunia Desemba 15 mwaka jana baada ya kupigwa risasi mgongoni na askari wa jeshi la polisi huku Lucas Edward akijeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi mkono wake na mbavu za kushoto wakati wakisubiri matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa, pamoja na mkutano huo wakazi wa mji wa Nzega wakaamua kuchanga fedha kwa ajili ya mafunzo ya mjane na mtoto wa marehemu kiasi cha shilingi milioni moja.