Mizengo Pinda
Waziri mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda amezitaka halmashauri zote nchini kuacha siasa katika suala la ujenzi wa maabara kwenye shule za sekondari na badala yake waongeze nguvu na kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kabla ya mwezi Juni mwaka huu ili wanafunzi waanze kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo.
Waziri mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika shule ya sekondari Songwe wilayani Mbeya ambako pia ametembelea na kukagua vyumba vitatu vya maabara ambavyo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.
Katika hatua nyingine Pinda ametemebelea na kuweka jiwe la msingi katika soko la kimataifa la Mwanjelwa jijini Mbeya ambako pia ameagiza ujenzi wa soko hilo ambao umechukua zaidi ya miaka mitano sasa, kuhakikisha unakamilika na wananchi wanaanza kulitumia kabla ya mwezi Juni mwaka huu huku akitaka wafanyabiashara waliokuwepo wakati soko hilo likiungua mwaka 2006 kupewa kwanza sehemu ya kufanyia biashara zao kabla ya watu wengine.
Meya wa jiji la Mbeya amesema kuwa ujenzi wa soko hilo umechelewa kukamilika kutokana na mkandarasi wa kwanza kufungua kesi mahakamani wakati akiondolewa, huku Kaimu Mkurugenzi wa jiji la Mbeya, Mussa Zungiza akidai kuwa ujenzi wa soko hilo la kisasa umezingatia tahadhari ya moto ili kuepusha matukio ya masoko kuungua moto ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara jijini Mbeya.
Ujenzi wa soko la mwanjelwa ulianza mwaka 2009 na ulitarajiwa kukamilika mwaka 2013 lakini haukukamilika na sasa unatarajiwa kukamilika Aprili 30, mwaka huu.