Sunday , 26th Nov , 2017

Nyota wawili wa klabu ya Azam FC, Shaaban Idd na Joseph Kimwaga, waliokuwa majeruhi  wanatarajiwa kurejea dimbani Januari mwakani wakati timu hiyo itakuwa inashiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar.

Mbali na kufanya programu ya mazoezi ya gym, Idd tayari ameruhusiwa kuanza mazoezi madogo madogo ya kucheza na mpira na kukimbia mwanzoni mwa wiki hii huku Kimwaga akiendelea na mazoezi ya gym aliyoanza mwezi mmoja uliopita.

Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, amesema wachezaji hao wapo kwenye kipindi cha mwisho cha tiba yao cha kuwarejesha katika hali yao ya kawaida ambapo Idd anaweza kurejea dimbani kuanzia Januari Mosi.

“Kimwaga kidogo kumetokea matatizo katika ukunjaji wa goti lake baada ya operesheni kwa hiyo sasa hivi bado anafanya mazoezi ya kukunja goti na pindi atakapokuwa ameweza kukunja goti vizuri naye ataruhusiwa kuanza kucheza mpira kidogo na kukimbia naye pia tutamtarajia itakapofika Januari Mosi atarudi tena kiwanjani kwenye ushindani,” amesema Mwanandi.

Idd anasumbuliwa na majeraha ya nyonga yake ya mguu wa kulia huku Kimwaga akisumbuliwa na goti la mguu wa kushoto kwa pamoja walifanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini.