Wednesday , 12th Sep , 2018

Ofisa Msajili wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Manispaa ya Kinondoni, Dickson Mbanga, amesema, kwa walemavu ambao hawataweza kufika kwenye usajili wa vitambulisho vya taifa umeandaliwa utaratibu wa kuwafuata majumbani.

Mmoja wa walemavu akiwa katika hatua ya mwisho ya upigaji picha ili aweze kupata kitambulisho cha utaifa katika mchakato wa utoaji wa vitambulisho vya utaifa kwa watu wenye ulemavu.

Mbanga amesema kuwa Manispaa ya Kinondoni imeanza usajili wa vitambulisho vya taifa kwa watu wenye ulemavu baada ya kubaini kundi hilo hukosa huduma nyingi za msingi kwa kutokuwa na vitambulisho hivyo.

"Tumeandaa utaratibu maalum kwa ajili yao tunataka kuona kila mlemavu anapata kitambulisho hiki kwa sababu ya umuhimu wake hasa kwenye huduma nyingine za msingi kama matibabu na mikopo," amesema Mbanga.

Akizindua usajili huo katika viwanja vya shule ya msingi Ndugumbi, leo Septemba 2, 2018, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo amesema utafanywa kwa siku tatu ukihusisha makundi yote ya walemavu.

Zipo huduma nyingi ambazo wenzetu hawa wamekuwa wanakosa kwa sababu ya ulemavu wao, niwaombe tu wajitokeze kwa wingi kujiandikisha," amesema Chongolo.

Hayo yanajiri ikiwa ni miaka miwili tangu kutolewa kwa tamko na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tazaniana, Dk. John  Magufuli la kuitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, (NIDA), kuhakikisha kila Mtanzania anapatiwa kitambulisho cha Uraia.