Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa amesema anafurahishwa na watu wenye maono na wanaopenda kuchukua maamuzi kuliko wale wenye kaliba ya kutaka kuweka rekodi pekee.
Mh. Lowassa amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa Helkopta ambayo ni mali ya Kanisa la Ufufuo na Uzima lililo chini ya Askofu Josephat GWAJIMA ambayo mbali ya shughuli za kikanisa, itatumika pia katika shughuli mbalimbali za kibinadamu wakati wa majanga, pamoja na kusambazia neno la Mungu.
Lowassa amebainisha kuwa Gwajima ni mmoja kati ya viongozi wenye maono ambao kimsingi ndiyo wanaohitajika kwa ajili ya ustawi wa jamii.
Lowassa pia ameahidi kumsaidia kwa maombi na njia nyingine Askofu Gwajima ili aweze kupata eneo la Tanganyika Pakers analolitumia kwa mahubiri ili ajenge kanisa kwa ajili ya waumini wake.
Kauli hiyo imefutia ombi la askofu ambaye amedai kuwa amesikia eneo hilo lipo katika mchakato wa kupatiwa mwekezaji.
Katika uzinduzi huo, Lowassa amesema kuwa hakwenda kutangaza nia na bado hajafikia maamuzi hayo, wakati ukifika ataweka wazi nia yake ya kugombea Urais mwakani.
Awali Gwajima alisema kuwa Helikopta hiyo ni moja kati ya nyingine mbili zinazotarajiwa mwakani kwa ajili ya kanisa na uokozi.
Amesema kuwa ameshawishika kuinunua baada ya kuona abiria waliokuwa katika meli ya MV Spice walivyopoteza maisha kutokana na kukosa msaada hali ambayo inawapata pia majeruhi wa ajali nyingine ambao wengi wao hufariki dunia wakiwa njiani kukimbizwa hospitalini.