Wednesday , 29th Aug , 2018

Jeshi la Polisi mkoani Kagera linamshikilia mwalimu Respicius Patrick wa shule ya msingi Kibeta, akituhumiwa kusababisha kifo cha mwanafunzi wa darasa la tano Siperius Eradius, ambaye alifariki akiwa njiani akipelekwa hospitali.

Siperius Eradius, enzi za uhai wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi amesema kuwa Patrick, ambaye ni mwalimu wa nidhamu anadaiwa kumpiga mwanafunzi huyo akihusishwa na upotevu wa mkoba wa mwalimu Herieth Gerard, uliokuwa na Shilingi elfu 75,000 na vitambulisho vyake.

Ollomi ameongeza kuwa kwa mujibu wa Baba wa mwanafunzi huyo, Justus Balilemwa, mtoto huyo alimchukua katika kituo cha watoto yatima cha Ntoma baada ya mama yake kufariki dunia akijifungua.

"Imeelezwa katika pochi kulikuwa na pesa taslimu Sh. 75,000, kitambulisho cha mpigakura, kitambulisho cha uraia, kadi ya benki na simu ya mkononi”, amesema Kamanda Ollomi.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kagera, Dkt. John Mwombeki, alikiri kupokea mwili wa mtoto huyo Agosti 27, mwaka huu saa mbili asubuhi na kusema mwili wake ulikutwa na majeraha yaliyoonyesha ni ya siku za nyuma kidogo.