
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa wizara yake inatarajia kuwasilisha bungeni muswada wa sheria ya wazee itakayolinda na kusimamia maslahi ya wazee nchini katika bunge lijalo la Septemba mwaka huu.
Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na baraza la mtandao wa mashirika ya wazee kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa mtandao huo uliofanyika mkoani Dodoma.
Amesema kuwa lengo kuu la muswada huo ni kuwawezesha wazee kuingia kwenye vyombo ya kutoa maamuzi nchini na nakutaka kila hospitali ya serikali kuwa na sehemu maalum ya kuwahudumia wazee.
Akizungumzia suala na matibabu bure kwa wazee, Mwalimu amesema kuwa kila hospitali ya serikali ni lazima iwe na sehemu maalum ya kuwahudumia wazee.
Wakizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo, Mzee Sebastian Bulegi ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika ya wazee Tanzania ameeleza kuwa mauaji ya wazee na vikongwe bado yanaendelea kutishia usalama wao.
Hata hivyo wazee walio wengi wanakabiliwa na changamoto ya kipato kutokana na wazee wengi kutonufaika na mfuko wa hifadhi ya jamii kwani wazee wengi waliajiriwa katika sekta isiyorasmi wakati wakiwa vijana ambapo ni asilimia 4 ya wazee wanaonufaika na mifuko hiyo. Serikali amesema inatambua kuwa wazee wote wataanza kulipwa pensheni ambayo itawasaidia kumudu gharama mbalimbali za kijamii.