Thursday , 7th Jul , 2016

Moto umetetekeza mabweni manne katika kituo cha kulea watoto ya Yatima na waishio katika mazingira magumu, cha Faraja kilichopo mkoani Iringa, na kusababisha hasara ya shilingi milioni 140.

Kituo cha Faraja kabla ya kuungua.

Moto huo ulioanza jioni katika kituo hicho kilichopo eneo la Mgongo, kata ya Nduli na kufanikiwa kuzimwa na kikosi cha zimamoto mkoani Iringa, umesababisha majeruhi mmoja alielazwa katika hospitali ya mkoa.

Moto huo unaosadikiwa kuanzia kwenye chumba kimoja wapo cha watoto wa kike, umeteketeza magodoro yote, vyombo vya kulia, nguo za wanafunzi zikiwemo sare za shule na vyakula vilivyohifadhiwa stoo.

Watoto zaidi ya 70 wanaohifadhiwa kituoni hapo sasa hawana mahala pa kulala na watalazimika kutafuta sehemu nyingine ili waweze kujisitiri wakati jengo lao hilo likifanyiwa matengenezo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza ametembelea eneo la tukio na kujionea uharibufu uliofanywa na moto huo na kisha kutoa msaada wa Magodoro na Mablanketi kwa watoto hao ili wapate sehemu ya kujihifadhi.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, kumpeleka Muhandisi atakaenda kuangalia namna bora ya kukarabati majengo hayo ili iwe rahisi kwa wanafunzi kutoka kipindi yanapotokea maafa.