Wednesday , 10th Dec , 2014

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amelitaka jeshi la polisi mkoani humo kutotumia nguvu pamoja na kufurumusha mabomu ya machozi kuwatimua wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga mara wanapoombwa na halmashauri ya jiji bila kupata maelekezo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha ziara yake ya ghafla katika wilaya ya Nyamagana, Mulongo amesema kamanda wa polisi wa mkoa huo, hatakiwi kuruhusu polisi wake kuwafyatulia mabomu machinga huku viongozi wa jiji wakiwa wamekaa ofisini bila kujishughulisha kusikiliza malalamiko yanayowakabili.

Aidha, Mulongo ameutaka uongozi wa halmashauri ya jiji la Mwanza kuhakikisha tatizo la uchafu linamalizwa ili kuliweka jiji hilo katika hali ya usafi zaidi.

Pia mkuu wa mkoa huyo amemtaka afisa afya wa jiji, Danford Kamenya na mwenyekiti wa kikosi kazi cha usafi wa jiji, Kaobwe Phidelis, kufanya mazungumzo ya amani na wafanyabiashara ndogondogo na kuwatafutia maeneo yaliyoboreshwa.