Thursday , 9th Jun , 2016

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA Patrobas Katambi amesema kwamba taifa ambalo linaendeshwa bila kufuata misingi ya kisheria kwa kushemu haki za binadamu na utawala bora ni hatari sana.

Katambi ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na East Africa Radio kuhusu kuzuiliwa kwa mikutano yao kwa sababu za kiusalama ikiwa ni pamoja na polisi kutawanya mkutano wa Chadema wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.

''Tulipewa barua ya kuturuhusu kufanya mkutano na kutuambia tuhakikishe tuna ulinzi na wakatuambia na wao wangetuunga mkono katika kuhakikisha ulinzi zaidi cha kushangaza wametupa taarifa tukiwa kwenye mkutano kwamba wamepata taarifa kutoka juu za kuzuia mkutano huo na kusababisha vurugu pamoja na mali baadhi ya watu kuharibika''- Amesema Patrobas

''Vifaa vya mkutano vilitoka Dar es salaam na vikafika Kahama na kufungwa siku moja kabla ya mkutano muda wote wangeweza kusema kama wamezuia mkutano kuliko viongozi tumeanza kupanda jukwaani ndipo tunaanza kutawanywa''- Katambi.

Aidha Katambi amesisistiza kwamba serikali ya Rais Dkt. John Magufuli ikubali kukosolewa kwa lengo la kutawala vizuri lakini kuzuia mikutano ya vyama ambavyo vipo kisheria na kikatiba ni kuminya demokrasia jambo ambalo wao hawatakubaliana nalo.