Tuesday , 31st May , 2016

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna Diwan Athuman, amesema watanzania washirikiane vema na jeshi la Polisi katika kutoa taarifa za kuwafichua wote wanaotenda ukatili wa mauaji ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Kamishna Diwani ameyasema hayo kwenye mahojiano maalum na East Africa Radio na kusema suala la vitendo vya mauji ya kuchinjwa na kukatwa mapanga watu ambayo yanaonekana kushamiri siku za karibuni nchini yanachangiwa na mambo mbalimbali baadhi ya sababau kwa mujibu wa kipelelezi zinaonyesha watu wanaofanya vitendo vya mauaji nchini ni ndugu wambao wanakuwa na imani za kishirikina,mauaji mengine ni ya visa mbalimbali vya madai, mengine ni ya tabia za kilevi na mengine ni mauaji ya kiuhalifu.

Amesema tayari jeshi la Polisi nchini limeshawakamata watuhumiwa wengi wa makosa hayo na kwa mujibu wa sheria za kipelelezi hawawezi kuwatangaza wahalifu hao hadharani ili kulinda uchunguzi zaidi kufanyika na tayari wameshapeleka kesi hizo mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa, wengine wameshahukumiwa vifungo vya maisha jela na wengine wanasubiri kunyongwa.

Amesema wameweka mikakati madhubuti ya pamoja katika kukazana kukemea vitendo hivyo visiendelee kutokea kwenye jamii zetu sambamba na viongozi wa dili na serikali kuungana kwa pamoja katika kuzuia suala hili lisiendelee kutokea nchini.